BAADA ya Televisheni ya
Star TV kutangaza kujitoa kurusha matangazo yao kupitia kingamuzi cha Star
Times, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema sheria na leseni ya
huduma, inazuia kuchukua hatua hiyo.
Hata hivyo, TCRA imesema
inafanya uchunguzi na leo itakutana na uongozi wa Star TV na Star Times,
kuzungumzia suala hilo ili hatua za udhibiti, zichukuliwe kuwezesha wananchi
kupata haki ya msingi ya kupata matangazo ya kitaifa kupitia televisheni hiyo.
Star TV walitangaza
kutoonekana kupitia Star Times siku chache zilizopita. Uchunguzi wetu umebaini
kuwa, jana waliwasilisha barua ya hatua hiyo kwa kampuni ya Star Times kupitia
mwanasheria wa kampuni yao.
Meneja Mawasiliano wa
TCRA, Innocent Mungy aliliambia HabariLeo jana kuwa na wao wamesikia
taarifa hiyo kupitia vyombo vya habari Lakini, alisema Sheria ya Mawasiliano ya
Elektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010, haitoi fursa kwa watu wenye
televisheni kujitoa ama kujiweka kwenye ving’amuzi watakavyo.
“Kwa ujumla chaneli zile
tano za kitaifa, zinapaswa kuonekana bure kwenye ving’amuzi vyote, nasi
tumesikia habari hizi na lazima tufanye uchunguzi, lakini pande zote mbili
pamoja na sheria, pia wanafungwa na mkataba wa huduma kwa jamii na matakwa ya
leseni,” alisema Mungi na
kuongeza:
“Sheria inawataka
wawe na makubaliano, huwezi kusema mimi najitoa, leseni ina matakwa yake lazima
yafuatwe. Lakini kesho (leo) tutawaita kujua kilichotokea ni nini na hatua
zaidi zitachukuliwa baada ya hapo”.
Aliwahakikishia wananchi
ni haki yao kupata matangazo kupitia televisheni ya Star TV, hata bila kulipia
ving’amuzi, kama ilivyo kwa televisheni nyingine nne za ITV, TBC, Channel 10 na
EATV.
Msaidizi wa Meneja wa Star
Times, Hellen Elisa alithibitisha kujitoa kwa Star TV. Alieleza ni kweli
walipokea barua mbili juzi, zikieleza kuhusu hatua yao hiyo kwamba wamejitoa
kwa matakwa yao.
“Walituletea barua jana
(juzi) kupitia mwanasheria wao wa kampuni, wao ni wamiliki wa chaneli, na sisi
tunahusika kurusha matangazo, jambo lolote kama hili likitokea lazima kwanza
kutii sheria, tumewasiliana na TCRA na wakubwa wetu wa kazi wametueleza kuwa
wanalishughulikia kwa karibu,” alisema Elisa.
Kwa upande wake, Msimamizi
wa masuala ya Ving’amuzi wa Sahara Media Group, wamiliki wa Star TV, Steve
Diallo alipoulizwa kwa simu kuhusu kujitoa kwao Star Times, alisema yeye si
Msemaji na kumtaka mwandishi kuwasiliana na watu wengine.
Miezi kadhaa iliyopita, Clouds TV nayo ilijitoa,
lakini ikarejea tena. Jana, Mkurugenzi wa Utafiti wa Redio Clouds FM, Ruge
Mutahaba alisema sheria inawabana wamiliki wa televisheni za kijamii
kujitoa na wanapaswa kuonekana katika ving’amuzi vyote.
No comments:
Post a Comment